Ijumaa 28 Novemba 2025 - 08:05
Ripoti Kuhusiana na Kuanza Rasmi Kongamano la Kimataifa la Kumuenzi Ayatullah Mirza Na’ini Huko Najaf Ashraf

Hawza/ Kongamano la kimataifa la kumuenzi Allama Na’ini limefanyika kwa ushiriki wa wanazuoni na watu mashuhuri kwenye Haram Tukufu ya Alawi, na katika hafla hiyo pia kumezinduliwa mkusanyiko wa juzuu 40 za athari za mtafiti huyu mashuhuri.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Kongamano la Kimataifa la kumuenzi mtafiti na allama mkubwa, Mirza Muhammad Hussein Na’ini, limefanyika Alhamisi, tarehe 6 Azar 1404 Hijria Shamsia, kwenye Haram Tukufu ya Alawi.

Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano wa Haram Tukufu za Alawi na Husseini, pamoja na uongozi wa Hawza za Kielimu za Qum, kwa lengo la kuthamini jitihada na huduma za marehemu huyo. Katika hafla hii walihudhuria wageni miongoni mwa wanazuoni na watu mashuhuri wa Hawza za Kielimu za Qum na Mashhad, wawakilishi wa Marjaa at-Taqliid, kundi la wanazuoni, wanavyuoni, wahadhiri wa vyuo vikuu, wataalamu, wanafunzi na walimu wa Hawza za Kielimu za Najaf Ashraf na Karbala tukufu, pamoja na wasimamizi, wadhamini na wawakilishi wa Haram Tukufu na maeneo matukufu ya ziara kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kwa mujibu wa ripoti hii: Mzungumzaji wa kwanza wa kongamano hili alikuwa Sayyid Isa Al-Kharsan, Katibu Mkuu wa Haram Tukufu ya Alawi, ambaye aliwasilisha ujumbe wa kuwakaribisha wageni kwa niaba ya Haram hiyo Tukufu. Baadaye, Ayatullah Sheikh Jaafar Na’ini, mjukuu wa marehemu Ayatullah al-Udhma Na’ini, kwa niaba ya familia ya Na’ini, alitoa shukrani zake kwa misaada na maelekezo yenye thamani ya Ayatullah al-Udhma Sistani katika kuunga mkono kufanyika kwa kongamano hili nchini Iraq, na pia akawashukuru wasimamizi wa Haram Tukufu za Alawi na Husseini (a.s) pamoja na wahudhuriaji wote kwa kushiriki kwenye tukio hili muhimu la kielimu.

Katika hatua inayofuata, Ayatullah Sayyid Munir Al-Khabbaz alichambua nafasi ya kielimu ya Mirza Na’ini katika mihimili mitatu: ubora wa urithi wake wa kielimu katika fiqhi na usuli, tofauti za mijadala ya kiusuli kati ya takrira za wanafunzi wake wakubwa kama marehemu Ayatullah Khu’i na Sheikh Hussein Hilli, pamoja na kuchunguza tofauti zilizopo kati ya misingi ya kifikra ya ijtihaadi ya Mirza katika masomo yake na maandiko yake binafsi, hasa katika risala aliyoiandika kuhusu vazi lenye hali ya kutiliwa shaka.

Baadaye, Sayyid Abbas Al-Husseini, Mkurugenzi wa Jumuia ya Kielimu ya Imam Hussein (a.s) inayohusiana na Haram Tukufu ya Husseini, alitoa hotuba na akamtaja marehemu mtafiti Na’ini kuwa ni “hazina kamili ya elimu”. Alikumbusha werevu wake, ustadi wake wa kifasihi, kina cha falsafa, upeo wa kielimu katika ilimu ya aqida (kalam), pamoja na ufahamu wake wa kina juu ya mabadiliko ya zama.

Alisisitiza: Kufufua na kuhuhisha upya haiba ya Mirza Na’ini si hatua ya kisherehe tu, bali ni uaminifu kwa mwanazuoni ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya fikra ndani ya Hawza na katika uamsho wa kijamii wa Ulimwengu wa Kiislamu. Pia alitangaza ushiriki wa kielimu wa jumuia hiyo katika kuandaa tafiti tatu kutoka katika urithi wa Na’ini ambazo zimejumuishwa ndani ya mkusanyiko huo.

Ayatullah Alireza A’raafi: Mirza Na’ini ni faqihi aliyeutengeneza Uislamu

Sehemu muhimu ya hafla hii ilihusishwa na hotuba ya kina aliyoitoa Ayatullah A’raafi, Mkurugenzi wa Hawza Iran. Mwanzoni, alimfafanua Mirza Na’ini kuwa ni “mmoja wa watu wakubwa zaidi wa kielimu na kisiasa wa zama za kisasa” na akafafanua sifa zake za kipekee katika mihimili mitatu:

1. Upeo wa akili na ubunifu wa kielimu

Ayatullah A’raafi, akirejea akili pevu na uchambuzi makini wa Mirza katika kukabiliana na mabadiliko ya kimawazo na kisiasa, alisema: Na’ini kwa umahiri wake katika fiqhi, usuli, kalam, Qur’ani, hadithi na fikra za kisiasa, aliunda haiba kamilifu na adimu, na kwa ubunifu wake katika ilimu ya usuli akaweka hatua mpya katika taaluma hiyo. Kwa mujibu wake, Mirza aliweza kuunganisha kwa mafanikio “asili ya ijtihaadi” na “ufahamu wa mabadiliko mapya ya zama”.

2. Nafasi yake kijamii na kisiasa

A’raafi akirejea ushiriki hai wa Mirza katika Harakati ya Tumbaku, Mapinduzi ya Kikatiba ya Iran, na Mapinduzi ya mwaka 1920 nchini Iraq, alisisitiza kuwa Na’ini alikuwa miongoni mwa waasisi wa uamsho wa kisiasa ndani ya Hawza za Kielimu, na dhidi ya ukoloni na kurudi nyuma, alichukua misimamo yenye nuru na athari kubwa. Aidha alisisitiza umuhimu wa kuupitia upya uzoefu wa Mapinduzi ya Kikatiba na athari zake katika Harakati ya Imam Khomeini.

3. Vipengele vya kimaadili na kiroho

Ayatullah A’raafi, katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, aligusia vipengele vya kimaadili na kiroho vya maisha ya mtafiti Na’ini, na akaongeza: “Leo kuliko wakati mwingine wowote, tunawahitajia wanazuoni wa aina hii; wanazuoni wanaoongoza jamii kwa elimu yao, maadili yao na hali yao ya kiroho.”

Uzinduzi wa mkusanyiko wa juzuu 40 za athari ya Allama Na’ini

Mwisho wa hafla hii, kulizinduliwa mkusanyiko wa kielimu wa juzuu 40 za athari ya mtafiti Na’ini, ambazo ni matunda ya juhudi za miaka miwili za Hawza ya Qum na Jumuia ya Kielimu ya Imam Hussein (a.s).

Kadhalika, Mkurugenzi wa Haram Tukufu ya Alawi, Sayyid Isa Kharsan, alifanya hafla ya kukabidhi bendera ya Mola wa Waumini, Amirul-Muuminin (a.s), kwa Hawza ya mji mtukufu wa Qum, ambapo bendera hiyo ilikabidhiwa kwa Ayatullah Alireza A’raafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, pamoja na wanazuoni wakubwa waliokuwepo hapo.

Inafaa kutajwa kwamba: Kongamano la Kimataifa la Allama Mirza Na’ini katika awamu yake ya kwanza lilifanyika tarehe 1 Aban 1404 Hijria Shamsia katika mji mtukufu wa Qum, kwa ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, na kwa hotuba maalumu ya Ayatullah al-Udhma Jaafar Subhani, pamoja na kuhudhuriwa na kundi la wanazuoni, walimu na wanafunzi wa Hawza za Kielimu, katika Chuo cha Kiislamu cha Imam Kadhim (a.s). Kisha kongamano hili liliendelea siku ya tatu ya Aban 1404 katika mji mtukufu wa Mashhad. Awamu ya mwisho ya kongamano hili pia itafanyika nchini Iraq, ambapo kikao chake cha kwanza kimefanyika huko Najaf Ashraf, na kikao cha mwisho kitafanyika tarehe 8 Azar 1404 huko Karbala Mualla.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha